Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu katika ofisi zetu ni muhimu watumishi wa Serikali kuwa na uelewa na ujuzi wa teknolojia za kisasa, ikiwemo Akili Unde.
Bw. Abdulla ametoa wito huo tarehe 23 Septemba, 2026 wakati akifungua mafunzo kuhusu Akili Unde kwa Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu teknolojia hiyo na matumizi yake katika utendaji kazi wao.
Amesema kuwa mafunzo haya ya siku tatu yanalenga kuongeza uelewa kuhusu mwelekeo wa maendeleo ya Teknolojia zinazoibukia kwenye uchumi wa kidijitali pamoja na umuhimu wa Akili Unde katika utendaji kazi wa kila siku.
Kwa upande wake, Kamishna wa Utafiti na Maendeleo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Meja Jenerali Michael Mumanga aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameishukuru Wizara ya Mawasiliano kwa kuleta mafunzo haya kwa viongozi hao na kwamba mafunzo haya yataongeza maarifa, uelewa na uwezo wa washiriki katika masuala ya teknolojia zinazoibukia ikiwemo Akili Unde.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kuendelea kujenga uwezo wa Taasisi za Serikali kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan Akili Unde, kwa ajili ya kuongeza ufanisi, ubunifu na kuimarisha utoaji wa huduma katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.