Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, wamemkamata dereva wa gari la Serikali aliyekuwa akiendesha akiwa amelewa, kitendo kinachodaiwa kuhatarisha usalama wa abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Dereva huyo alikamatwa wakati wa ukaguzi wa mabasi uliofanyika jana mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha usalama barabarani na kudhibiti ajali.
Akizungumza baada ya kukamatwa kwa dereva huyo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Kilimanjaro, ACP Nassoro Sisiwayah, amesema Jeshi la Polisi halitavumilia madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, hususan wanaoendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa.
Ameongeza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya madereva wote wenye tabia kama hiyo, akisisitiza kuwa vyombo vya dola vimejipanga kudhibiti vitendo vinavyoweza kusababisha ajali na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Chanzo; Nipashe