Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kusini, Mtwara imewahukumu kunyongwa hadi kufa Mapacha wawili Wakulima Wakazi wa Kijiji cha Mraushi A Wilayani Masasi ambao ni Daniel Stephen Seif (Kurwa) (24) na Daniford Stephen Seif (24) (Doto), baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya Mama yao Mzazi.
Wawili hao wote kwa pamoja walitenda kosa hilo tarehe 15.12.2024 Katika Kijiji cha Mraushi A kwa kumpiga Mama yao Mzazi aitwae Upendo Methew (42) Mkazi wa Kijiji cha Mraushi A kwa kutumia jembe na mwichi na kumsababishia majeraha yaliyopelekea kifo chake ambapo wawili hao walikiri Mahakamani kuwa ni kweli walitekeleza mauaji hayo ya kikatili.
Imeelezwa kuwa Mapacha hao walikuwa wanamtuhumu Mama yao kuwa anawaloga ambapo tukio la mwisho ni pale Pacha mmoja alipokuwa anakosa nguvu za kushiriki tendo la ndoa na Mke wake (uume ulishindwa kusimama) na hata alipojaribu kwenda nje ya ndoa nako hali ikawa hivyohivyo.
Baada ya kuona tatizo hilo likiendelea wawili hao walikwenda kwa Baba yao kumueleza ambaye aliwapeleka kwa Mganga ambaye aliishia kuwaambia kuwa Mama yao ndiye amewaroga kwa kile kinachoaminika kuwa hakutaka wawili hao waishi na Wake zao ambapo baada ya kuambiwa hivyo walirudi nyumbani na kuchukua mwichi na silaha nyingine na kuanza kumshambulia Mama yao hadi kupelekea kifo chake.
Chanzo: Millard Ayo