Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania October 29 (kesho) yamekamilika huku Watanzania 37,647,235 ambao wamejiandikisha wakitarajia kupiga kura kumsaka Rais mmoja kati ya Wagombea 17 wa nafasi ya Urais, kuwapata wabunge kutoka katika majimbo 270, pamoja na madiwani katika kata 3945.
Taarifa hiyo ya INEC imetolewa leo Jumanne Oktoba 28, 2025 na Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele siku moja
kabla ya uchaguzi mkuu huku akisisitiza watendaji wa vituo tayari wamepatiwa mafunzo na taratibu zote za uchaguzi
zimekamilika kwa mujibu wa sheria.
“INEC imekamilisha maandalizi yote ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, tunawaomba Watanzania wote wajitokeze kwa amani, kwa kufuata sheria na kanuni za uchaguzi, amani ya nchi yetu ni jukumu letu sote,” amesema Jaji Mwambegele.
Katika taarifa yake, Jaji Mwambegele ametoa maelekezo 10 muhimu ambayo wapiga kura wote wanapaswa kuyazingatia
siku ya uchaguzi.
Kwa wapiga kura wasiokuwa na picha, Jaji Mwambegele
amesema wapiga kura ambao majina yao yapo kwenye Daftari la Kudumu lakini picha zao hazionekani, wataruhusiwa kupiga kura endapo taarifa nyingine kwenye kadi zitakuwa sahihi.
“Kwa wapiga kura waliopoteza au kuharibu kadi zao
wataruhusiwa kutumia kitambulisho cha Taifa (Nida), leseni ya udereva, au pasi ya kusafiria kuthibitisha utambulisho wao,” taarifa hiyo imeeleza.
Chanzo; Bongo 5