Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia na linaendelea kumuhoji Fahima Twaibu (19), msaidizi wa kazi za nyumbani kwa tuhuma za kutupa kichanga chenye jinsia ya kike, kinachokadiriwa kuwa na saa mbili tangu kuzaliwa.
Msaidizi huyo wa kazi za nyumbani mkazi wa Mtaa wa Balyehela wilayani Ilemela anadaiwa kufanya tukio hilo Desemba 25, 2025 saa 11.00 alfajiri.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatatu Desemba 29, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, mtuhumiwa Fahima Twaibu anadaiwa kutupa kichanga hicho muda mfupi baada ya kujifungua kwenye paa la nyumba inayomilikiwa na Emmanuel Muruli, ambaye ni fundi wa kuchomelea vyuma na mkazi wa Balyehela.
Mutafungwa amesema askari polisi walifika eneo hilo na kufanikiwa kuokoa maisha ya kichanga hicho kwa kushirikiana maofisa wa ustawi wa jamii pamoja na wananchi wa eneo hilo, na kukifikisha katika Hospitali ya Mkoa Sekou-Ture kwa matibabu.
"Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtuhumiwa ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Vitendo vya ukatili kwa watoto ni kosa la jinai na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo," amesema Mutafungwa.
Chanzo; Mwananchi