Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam imeahirisha Kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa (CHADEMA), Tundu Lissu hadi Novemba 3, 2025, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuendelea kutokana na kukosekana kwa Shahidi.
Wakili wa Serikali Mkuu Renatus Mkude aliieleza Mahakama kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa tayari umeshatoa ushahidi kupitia mashahidi watatu, lakini shahidi wa tatu, Mkaguzi wa Polisi na Mtaalamu wa Uchunguzi wa Kielektroniki Samwel Kaaya, alishindwa kuwasilisha vielelezo vyake vya flash disk na memory card baada ya Mahakama kukataa kuvipokea.
“Kwa sasa hatuna shahidi mwingine aliye tayari kutoa ushahidi kwa kuwa waliopangwa wanatoka nje ya Dar es Salaam na wanahitaji maandalizi zaidi. Kwa mujibu wa kifungu cha 302 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), tunaomba ahirisho,” alisema Mkude.
Kwa mujibu wa Wakili huyo wa Serikali, tarehe 3 Novemba 2025 ilikuwa tayari imepangwa katika ratiba ya kesi hiyo, hivyo aliomba shauri hilo liendelee siku hiyo.
Hata hivyo, Lissu alipinga ombi hilo la kuahirishwa akidai kuwa sababu zilizotolewa na upande wa Jamhuri hazina msingi wa kisheria.
Kutokana na hatua hiyo, Jaji Ndunguru, alisema Mahakama imezingatia hoja za pande zote mbili na kubaini kuwa ombi la kuahirisha lina msingi wa kisheria kwa kuwa upande wa mashtaka haujawahi kukosa shahidi tangu shauri lianze, hivyo kesi inaahirishwa hadi Novemba 3, 2025.
Chanzo: Millard Ayo