Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imekamata kilo 1,232 za nyama zilizoisha muda wake kwenye moja ya vyumba vya kuhifadhia bidhaa hiyo katika Kampuni ya JM Investment iliyopo Fuoni Ijitimai, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Miongoni mwa kilo hizo, vipo vipapatio vya kuku boksi 55, kuku paketi 254, vidali vya kuku paketi 58 na nyama ya ng’ombe paketi 12.
Akizungumzia hilo leo, Desemba 22, 2025, Mkaguzi wa Chakula kutoka ZFDA, Dk Thamra Khamis Talib, amesema wakati maofisa hao wakifanya ukaguzi wa kawaida waligundua bidhaa hiyo ikiwa imehifadhiwa huku ikiwa katika vifungashio visivyo vya asili.
Amesema kubadilishwa kwa vifungashio kunahusisha kampuni hiyo kubadilisha tarehe ya mwisho ya matumizi, jambo ambalo si sahihi.
Amesema bidhaa hiyo itabaki chini ya ZFDA kwani si salama kwa matumizi ya binadamu, na mmiliki wa bidhaa hiyo atachukuliwa hatua za kisheria kwa kushindwa kumlinda mtumiaji.
Chanzo; Mwananchi