Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikihoji alipo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche, familia ya kiongozi huyo imetoa muda wa siku moja kwa Jeshi la Polisi kueleza alipo ndugu yao kabla hawajaamua kumtafuta wao wenyewe kwa kushirikiana na wananchi.
Uamuzi huo umefanywa na familia hiyo kufuatia kuwepo wa taarifa kuwa Heche alisafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Tarime lakini hadi sasa bado hajafikishwa na wala hawana taarifa kuhusu ndugu yao huku wakidai kuwepo kwa danadana kutoka mamlaka mbalimbali.
Heche alikamatwa jana Oktoba 22, 2025 jijini Dar es Salaam katika viunga vya Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, alipokwenda kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.
Kabla ya kukamatwa, Idara ya Uhamiaji Makao Makuu, ilitoa taarifa ikidai kwamba Heche alivuka mpaka kinyume cha sheria, madai ambayo Heche mwenyewe alikanusha na kudai kwamba alikuwa nyumbani kwake Tarime mkoani Mara.
Leo, Oktoba 23, 2025, familia ya Heche iliyopo Kijiji cha Ketagasembe wilayani Tarime, imesema wameamua kutoa muda huo ili kuonyesha namna gani walivyo wavumilivu na kwamba hawataki kuzua taharuki yoyote.
Mdogo wa Heche, Chacha Heche amesema familia haiko tayari kuona ndugu yao akipoteza maisha bila sababu ya msingi kwani wanaamini kuwa ndugu yao hana makosa ya aina yoyote, zaidi amekuwa mstari wa mbele kudai haki na demokrasia kwa ustawi wa nchi na watu wake.
Mwananchi ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, kama kiongozi huyo wa Chadema kapelekwa Mara amesema hana taarifa hizo na Mara ina mikoa miwili.
Chanzo: Mwananchi