Kesi ya maombi ya dharura namba 24511 ya mwaka 2025 yaliyofunguliwa na Wakili Peter Kibatala dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) na wenzake wanne (4) imesikilizwa leo Alhamisi Oktoba 09 2025 katika Mahakama kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es salaam ambapo kesi hiyo imekuja kufuatia madai ya kutekwa kwa Mwanasiasa Humphrey Polepole.
Pamoja na mambo mengine katika wasilisho lake Mahakamani hapo leo, Wakili Peter Kibatala ameiomba Mahakama kutoa amri ya haraka ili wajibu maombi wamlete Mahakamani mleta maombi (Humphrey Polepole) leo hii wakati wanasubiri kusikiliza hoja za pande zote mbili (2)
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Faraja Nguka ameieleza Mahakama kuwa maombi hayo hayatekelezeki kwakuwa kiapo kilichowasilishwa Mahakamani hapo na Wakili wa mleta maombi (Peter Kibatala) hakijaonesha wazi ni nani hasa ambaye amemshikilia Humphrey Polepole, lakini pia ameendelea kusema kuwa kupitia kiapo hicho Wakili anakiri kwamba Mteja wake amechukuliwa na Watu wasiojulikana na kwamba hadi sasa haijulikani alipo.
Sambamba na hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Faraja Nguka ameieleza Mahakama kuwa kupitia kiapo hicho, Wakili Peter Kibatala amedai kuwa ana mashaka kwamba mleta maombi anashikiliwa na mjibu maombi namba tano (5) katika kesi hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZPC).
Katika maelezo yake KIbatala amesema amelazimika kuweka umahususi kwa Mjibu maombi wa tano kufuatia taarifa za awali alizozipata kutoka kwa ndugu wa Humphrey Polepole, akiwemo Godfrey na Augusto Polepole ambao taarifa zao na madai yao yameenea kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na Vyombo vya habari.
Baada ya majibizano kadhaa ya kisheria na maombi yaliyowasilishwa na pande zote mbili, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo ameihairisha kwa muda hadi saa 8 mchana ambapo atatoa uamuzi kuhusiana na maombi hayo.
Chanzo: Millard Ayo