Wivu wa kimapenzi umesababisha vifo vya watu wawili mkoani Mwanza, baada ya tukio la mauaji lililotokea wilaya ya Magu. Desemba 27 mwaka huu ambapo Marietha Kalafala (33), mfanyakazi wa Kiwanda cha Ziwa Steel na mkazi wa Kitongoji cha Mwabuyi, aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali katika shingo, mgongo na paji la uso na mwili wake kisha kutupwa kwenye shamba la mahindi.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mauaji hayo yalifanywa na mpenzi wake, Wilbert Yona (34), mfanyakazi wa Kiwanda cha Ziwa Steel. Baada ya tukio hilo, Desemba 28 majira ya saa 3 asubuhi, Wilbert alijinyonga ndani ya nyumba ya kulala wageni iliyopo Kata ya Nyanguge, Wilaya ya Magu, ikidaiwa ni ili kuepuka hatua za kisheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mtafungwa, amesema miili ya marehemu wote wawili imehifadhiwa katika Kituo cha Afya Lugeye kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu na kisha itakabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi.
Chanzo; Nipashe