"Kwa niaba ya wanajimbo Kuu la Songea tunapenda kutoa taarifa kwamba Padri Camillus Nikata wa Jimbo Kuu la Songea, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Mwanza, haonekani wala hapatikani kwenye simu yake."
"Padri Nikata alikuwa ametokea Dodoma kwenye mafundisho ya moyo ya mapadri wanaofundisha katika Vyuo vikuu vya TEC, akiwa na mhadhiri mwenzake, ambaye ni Padri wa Jimbo hili."
"Hapa Songea alikaa katika nyumba ya mapadri, St. Vianney. Alikuwa amepanga kusafiri kwenda Mwanza tarehe 08 Oktoba 2025, siku ya Jumatano asubuhi, kwa basi la SUPERFEO, na tiketi alishainunua kwa mtandao."
"Lakini siku hiyo ya Jumatano mchana tulianza kuhisi kwamba hajasafiri kwenda Mwanza kwani katika chumba chake kilichokuwa kimefungwa ilionekana mizigo yake ambayo alikuwa ameiandaa kwa ajili ya safari."
"Mtumishi wa nyumba ya mapadri alishangaa kwamba mzigo ambao Padri ilitakiwa auchukue toka kwake haukuchukuliwa. Pia mlango wa chumba ulifungwa, lakini ufunguo haukurudishwa kwa mtumishi."
"Baada ya kuona hayo tulianza kumtafuta kwa simu na kwa kuulizia kwa watu aliokaa nao katika nyumba ya mapadri. Hata hivyo hatukufaulu kupata chochote, maana hakupatikana kwa simu na watu hawakujua alikokwenda."
"Kule Mwanza alikotakiwa kwenda, nako haonekani na hapatikani. Ofisi ya SUPERFEO ilidhihirisha kuwa Padri Nikata alinunua tiketi lakini hakusafiri kwa basi lile."
"Baada ya kushindikana kwa jitihada za kumtafuta kila mahali ambapo tulidhani angeweza kuwepo, tumepeleka taarifa Polisi."- Damian Dallu
Askofu Mkuu wa Songea
Chanzo: Nipashe