Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe wamelalamikia ongezeko la mamba ndani ya Ziwa Viktoria na kuleta madhara kwa wananchi wa wilaya hiyo baada ya miezi mitatu iliyopita matukio zaidi ya matano kuripotiwa ya wananchi kuvamiwa, kushambuliwa, kuuliwa na kubebwa na mamba pamoja na viboko.
Hayo yameelezwa na madiwani wa kata za Kagunguli, Ngoma na Igala katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe jana mjini Nansio.
Akizungumzia matukio hayo, Diwani wa Kata ya Kagunguli, Paschal Ludomya amesema tukio la hivi karibuni ni la mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Colnel Maghembe aliyeshambuliwa na mamba saa 11 alfajiri wakati akioga ziwani kwa ajili ya kujiandaa kwenda shule, na mpaka sasa mwili wake haujapatikana.
“Mwanafunzi huyo kwa maelezo ya wazazi ni kwamba aliamka alfajiri ya saa 11 kwa ajili ya kujiandaa kwenda shuleni, makazi yao ni karibu na mwalo hivyo alienda kuoga akiwa na mdogo wake sasa wakati anamalizia kuoga ili avae aondoke kwenda nyumbani yule mamba akamnasa mguu wake, mdogo wake akakimbia kwenda kutoa taarifa nyumbani lakini wazazi walipokuja wakakuta mamba ameshatokomea na yule mtoto,” amesema Ludomya.
Diwani huyo ameiomba serikali kuimarisha doria ya kuwasaka mamba na viboko ambao wamekuwa wakihatarisha maisha ya wananchi wanaozunguka maeneo ya ziwa hususan kata yake ambayo sehemu kubwa inazungukwa na maji ya Ziwa Viktoria.
Naye, Diwani wa Kata ya Ngoma, Mugeta Nyagabona amesema kutokana na tishio la mamba hao wananchi wa kata hiyo wamepitisha mchango wa Sh. 1,000 kwa kila mmoja kwa ajili ya kupambana na wanyama hao ikiwemo kuwawinda na kuwanasa ziwani na tayari wamefanikisha kuua mamba wanne na viboko watano.
Akitolea ufafanuzi wa changamoto ya wanyama hao, Mkuu wa Kitengo Cha Maliasili na Hifadhi ya Mazingira Wilaya ya Ukerewe, Goodluck Mtigandi amesema ongezeko hilo la mamba ni kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambapo wanahama kutoka korido la mbuga ya Serengeti na kuingia Ziwa Viktoria.
Chanzo; Nipashe