Kipindi cha The Dark, mikasa na matukio kwa wiki hii, kimekuletea kisa cha kijana wa mtaani, Gidion Cosmas, ambaye amedai ameishi kwa kulala nje kwa kipindi cha miaka miwili, akitegemea kuosha vioo vya magari barabarani na kuomba ili ajipatie pesa ya kula.
Kijana huyo amedai kuwa Baba yake alifariki na kulelewa na Mama yake pamoja na Baba wa kambo. Alikuja Dar es Salaam miaka miwili iliyopita akiwa chini ya basi (chases), akidai alikimbia vipigo vya Baba yake wa kambo.
Gidion amedai kwa sasa amechoka kulala nje, na anawaomba Watanzania kumpeleka gereji na kumtafutia makazi ili aanze kujipanga kimaisha, kwani anaamini siku moja atakuja kuwa Baba.
Licha ya Serikali, kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, kufanya kazi kubwa ya kuwaondoa watoto hawa mitaani na kuwaunganisha na ndugu zao, huku wengine wakitafutiwa ujuzi, bado kuna vijana wengine mitaani ambao wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku, hali ambayo inahitaji ushirikishwaji wa jamii katika kutatua kero hiyo na kujenga jamii iliyo bora.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu imewaunganisha na familia zao watoto 1,346 nchini waliokuwa wakiishi mitaani katika kipindi cha kati ya Julai 2021 hadi Aprili 2024.
Watoto hao ni miongoni mwa 6,459 waliobainika wakati wa zoezi la utambuzi wa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani, huku 816 wakiunganishwa na mafunzo ya stadi za maisha na kupatiwa mitaji pamoja na vifaa vya kazi.
Watoto wengine 3,427 walipewa vifaa vya shule na mahitaji mbalimbali, 273 walipatiwa huduma ya kuimarisha uchumi wa kata, huku 597 wakiendelea kupatiwa huduma kwenye vituo maalumu na makao ya watoto, wakiandaliwa kwa ajili ya utengamano.
Chanzo; Bongo 5