Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Ng’ombe 22 Wafa Katika Mazingira ya Kutatanisha

Ukisikia kulala tajiri na kuamka maskini ndiyo hii sasa!

Ng’ombe 22 wanaomilikiwa na mfugaji Alex Idege, mkazi wa Kijiji cha Kasingili, Kata ya Ilola wilayani Shinyanga, wamekufa ghafla wakiwa zizini huku chanzo kikiwa na utata.

Inaelezwa kuwa tukio hilo limetokea Desemba 18 ambapo ng'ombe walirejea kutoka malishoni na kuingizwa zizini.

Ilipofika majira ya saa 10 alfajiri, mmiliki wa mifugo hiyo amesema alisikia ng’ombe wakilia ambapo alitoka nje na kumulika zizi, akaona mifugo ipo salama ndipo akarudi kulala.

Ilipofika saa 11 alfajiri, kijana aliyekuwa amefika kwa ajili ya kufunga ng’ombe ili waende kulima alibaini kuwa baadhi ya mifugo hiyo imekufa na kutoa taarifa.

Idege amesema alipofika zizini kwa mara ya pili alikuta ng’ombe sita tayari wamekufa huku wengine wakiwa katika hali mbaya, na kadri muda ulivyopita idadi ya waliokufa iliendelea kuongezeka hadi kufikia ng’ombe 22, huku wakibaki ndama watatu pekee ambao hawakupelekwa malishoni.

Ameeleza kuwa mifugo yake huwa inalishwa eneo moja kwa muda mrefu, hivyo hajaridhishwa na maelezo aliyopata kutoka kwa mtaalamu wa mifugo kwamba huenda walikula majani yenye sumu.

Diwani wa Kata ya Ilola, Kisena Fred, amesema amesikitishwa na tukio hilo na kuomba uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo cha vifo hivyo.

Ameongeza kuwa endapo chanzo kitabainika kuwa ni ugonjwa, hatua za haraka zichukuliwe ili kuzuia kuenea kwake na kuathiri mifugo ya wafugaji wengine.

Amesema mfugaji huyo amepoteza rasilimali muhimu aliyokuwa akiitegemea kiuchumi kupitia kilimo na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, hivyo anahitaji kufarijiwa.

Aidha, ameeleza kuwa amempatia msaada wa shilingi laki moja kama pole, huku akisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa kina kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo.

Kwa upande wake, Afisa Mifugo wa Kata ya Ilola, Daniel Jilala, amesema tayari sampuli za mifugo hiyo zimechukuliwa na uchunguzi unaendelea. Hata hivyo, uchunguzi wa awali unaashiria kuwa ng’ombe hao huenda walikula majani yenye sumu.

 

 

Chanzo; Global Publishers

Kuhusiana na mada hii: