Upo katika eneo gani kwa sasa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani na Visiwa vya Mafia na Unguja na Pemba, je hapo ulipo umefikiwa na mvua ambazo zinakupa maswali kama ni za msimu wa vuli au ni zile zilizo nje ya msimu?
Usipate tabu juu ya mvua hizi, kwani tayari Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini TMA imeshatabiri juu ya uwepo wa vipindi vifupi za mvua kubwa zinazochangiwa na athari za uwepo wa Kimbunga Chenge ambacho hadi kufikia Jumamosi ya Oktoba 25 kilikuwa Kilometa 1,280 Mashariki mwa Pwani ya Kisiwa cha Mafia.
Hata hivyo kimbunga hicho kimeendelea kusalia baharini na kusogea kuelekea ukanda wa Pwani ya Tanzania huku kikipungua nguvu yake hali inayosababisha vipindi vichache vya mvua kubwa kujitokeza katika mikoa tajwa na maeneo ya jirani.
Hivyo kutokana na mwelekeo huo wa Kimbunga Chenge, jipange na mvua hizo kubwa ambazo zitanyesha katika baadhi ya maeneo hivyo watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wakitakiwa kuchukua tahadhari huku wakishauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA.
TMA pia inaendelea kufuatilia mwenendo wa Kimbunga Chenge na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.
Chanzo: Clouds Media