Anna Mary ambaye ni Mama Mzazi wa Mwanasiasa Humphrey Polepole amefika katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es salaam asubuhi hii ambako inatarajiwa kuanza kusikilizwa kwa maombi ya kesi juu ya kutekwa kwake maombi ambayo yalipelekwa na Wakili Peter Kibatala kuiomba Mahakama Kuu chini ya hati ya dharura, itoe amri ya kwamba Polepole afikishwe Mahakamani ama Mamlaka husika ziseme yupo wapi.
Kwa mujibu hati iliyosajiliwa baada ya kupokelewa kwa maombi hayo na kupewa namba 24514 ya mwaka 2025, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Salma Maghimbi ambapo katika maombi hayo Kibatala ameiomba Mahakama iingilie kati mara moja akidai kuwa Polepole alitekwa nyara alfajiri ya Jumatatu, tarehe 6 Oktoba 2025 kutoka katika makazi yake yaliyoko eneo la Ununio, Wilaya ya Kinondoni, Dar es salaam na Watu waliotajwa kuwa ni Askari wa Jeshi la Polisi la Tanzania.
Katika hati hiyo ya dharura Wakili Kibatala ameieleza Mahakama kuwa Polepole hajawahi kushtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika Mahakama yoyote, na kwamba kwa sasa inaaminika anashikiliwa katika eneo lisilojulikana na maafisa wa Jeshi la Polisi.
Maombi hayo yamewasilishwa dhidi ya wajibu maombi watano akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Afisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (RCO) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (RPC).
Chanzo: Millard Ayo