Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Amani Golugwa amesema hadi sasa hawajui ni wapi alipo Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho John Heche licha ya kuambiwa na Jeshi la Polisi kuwa amepelekwa Tarime, Mara.
Golugwa ameyasema hayo nje ya Mahakama Kuu ya Tanzania Masijala Ndogo ya Dar es salaam baada ya kuahirishwa kwa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wao, Tundu Lissu.
“Siku ya jana Makamu Mwenyekiti wakati anaingia katika geti la Mahakama Kuu hapa alikamatwa na kuwekwa katika mikono ya Jeshi la Polisi na alipelekwa Central Police na taarifa tulizozipata kutoka kwa Mawakili wetu walijulishwa kwamba ni kweli wamemchukua na kwamba wanamsafirisha kuelekea Tarime Mara lakini hadi sasa yakiwa yamepita masaa 24 tumefuatilia Wilayani Tarime na Mkoani na Mawakili wamekwenda na kuuliza iwapo Heche amefikshwa lakini tumeambiwa hajafikishwa” - Amani Golugwa.
AyoTV imelitafuta Jeshi la Polisi kwa ajili ya kutaka kufahamu kuhusu madai yaliyotolewa na CHADEMA lakini haijafanikiwa, jitihada za kuendelea kuutafuta ufafanuzi kutoka kwenye Jeshi hilo zinaendelea.
Chanzo: Millard Ayo