Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeiamuru Kampuni ya UDA Rapid Transport Ltd kumlipa fidia ya shilingi milioni 88.8 Frank Zebaza, baada ya kugongwa na basi la mwendokasi. Aidha, Mahakama imembaini dereva wa basi hilo, Hafidhi Ally, kuwa alikuwa akiendesha kwa mwendo hatarishi na kumuamuru pia kumlipa Zebaza fidia ya shilingi milioni 10.
Hukumu hiyo ilitolewa Desemba 19, 2025 na Jaji Griffin Mwakapeje, kufuatia kesi ya madai namba 28992 ya mwaka 2024 iliyofunguliwa na Frank Zebaza dhidi ya UDA Rapid Transport Ltd, dereva Hafidhi Ally, Shirika la Taifa la Bima (NIC) pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Katika kesi hiyo, mlalamikaji alikuwa akiomba fidia ya jumla ya shilingi milioni 600 kwa madhara aliyoyapata.
Katika madai yake, Zebaza aliomba alipwe shilingi milioni 350 kama fidia maalumu kwa gharama za matibabu na matumizi mengine yanayotokana na ajali hiyo, shilingi milioni 150 kama fidia ya jumla kwa maumivu na mateso aliyopitia, pamoja na shilingi milioni 100 kama fidia ya adhabu.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mwakapeje alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani unaonesha wazi kuwa mlalamikaji alipata majeraha makubwa yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji mkubwa, na kwamba hadi sasa anaendelea kukumbwa na athari za kudumu katika mfumo wa fahamu na hisia, hali iliyopunguza uwezo wake wa kufanya kazi.
“Majeraha haya yalimlazimu mlalamikaji kuhama kutoka Mbezi Makondeko kwenda Mikocheni kwa sababu za usalama na uangalizi wa kiafya,” alisema Jaji Mwakapeje.
Aliongeza kuwa kutokana na hali yake kiafya, Zebaza ameshindwa kuendelea na shughuli zake za awali kama mwanamuziki na mpishi, hali iliyosababisha kupoteza uwezo wake wa kujipatia kipato.
Mahakama ilisisitiza umuhimu wa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazosababisha madhara makubwa kwa wananchi.
Chanzo; Global Publishers