Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Makamu Mwenyekiti Taifa, John Heche anashikiliwa kwenye mahabusu ya Jeshi la Polisi Mtumba, Dodoma ambako leo ljumaa, October 24,2025 alihojiwa na Idara ya Uhamiaji mbele ya Wakili wa Chama na Kaka yake akituhumiwa kuvunja sheria za uhamiaji kwa kile walichosema alivuka mpaka wa Tanzania na kuingia Kenya bila kufuata taratibu.
Taarifa iliyotolewa leo October 24,2025 na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi CHADEMA, Brenda Rupia imenukuliwa ikieleza yafuatayo “pamoja na kosa hilo alilotajiwa ambalo lina dhamana, Jeshi la Polisi limekataa kumpa dhamana likisema kuwa kuna maelekezo kutoka juu kuwa aendelee kubaki Mahabusu”
“Heche alikamatwa na Jeshi la Polisi juzi Jumatano kwenye geti la Mahakama Kuu Masijala ya Dar es salaam kabla ya kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi (Central), Dar es salaam kisha Jeshi hilo likasema linamsafirisha kumpeleka Polisi Tarime Mkoani Mara, kuendelea kumshikilia Heche kinyume cha Sheria ni muendelezo wa mpango wa Serikali ya CCM chini ya Rais Samia kuwakamata Viongozi Wakuu wa Chama na kuwaweka kizuizini mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 29 Oktoba, 2025” imeeleza taarifa ya CHADEMA.
Chanzo: Millard Ayo