Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesimulia kisa cha mkazi wa Arusha ambaye amelizwa kiasi cha takriban Sh600 milioni na kijana aliyemuamini akamchukulie mkopo.
Kutokana na kisa hicho, Dk Mwigulu amemuagiza Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Justine Masejo, kijana huyo apatikanae na ikiwezekana ukoo wake wote ukamatwe.
Dk Mwigulu ameeleza hayo leo Desemba 29,2025 akizungumza na wananchi, baada ya kukagua ujenzi wa soko na stendi ya Bunju B jijini Dar es Salaam.
Dk Mwigulu amesema mama huyo anasumbuliwa kulipa mkopo huo wakati kijana aliyeuchukua haguswi.
“Nimemuelekeza RPC amsake huyo kijana akamatwe hata wakikamatwa ukoo mzima wakamatwe walipe fedha zile, hawezi mama maskini anakosa pa kukaa wakati yule aliyekula fedha anatembea mkanda nje,”amesema.
Amesema kwa mambo hayo wapo watu wanasema Waziri Mkuu anafoka akiahidi kuwa hawezi kuwaimbia mapambio watu wa namna hiyo. Dk Mwigulu ameagiza vyombo vyote vya dola Mkoa wa Arusha muhusika wa tukio hilo asakwe na kukamatwa popote alipo.
Chanzo; Mwananchi