Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Joseph Mlola, ametaka Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya zitumike kuwa chachu ya kuzika tofauti na kujenga utayari wa kuanza upya, akisisitiza kukomeshwa kwa ufisadi, ukatili, ulafi, ibada za uongo, hasira na fitina.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi Desemba 25, 2025 wakati wa Ibada ya kitaifa iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Bikira Maria Mshindani-Kigoma.
Amesema ni muhimu kuwa tayari kuanza upya katika maisha na daima tusikubali kubaki sehemu moja, kwani binadamu anapaswa kubadilika.
“Kama tulikuwa na mahusiano mabaya, hatuelewani tuanze maisha mapya, kama tulikuwa na tabia mbaya tuanze upya, Krismasi ni mwanzo mpya. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo ni mwanzo mpya wa maisha,” amesema.
Ametaka watu kuwa tayari kuzika tofauti kwa kuhakikisha visababishi vya kutofanana na Mungu vinang’olewa ikiwemo ukatili, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada za uongo, uchawi, hasira, fitina, uzushi, husuda, ulevi na ulafi.
Ameitaka jamii kushikamana na masuala ya kiroho yatakayoipeleka katika uzima, upendo, haki, amani, uvumilivu, furaha, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi.
Chanzo; Mwananchi