Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imewakamata watu wanne wanaodaiwa kukutwa wanatengeneza biskuti za bangi wakiwa kwenye sherehe ya kuzaliwa mwenzao, maarufu ‘house party’.
Watuhumiwa hao wanne ambao wote wana umri wa miaka 26 wanadaiwa kuwa wanafunzi wa chuo kikuu na walikusanyika katika nyumba hiyo iliyopo eneo la Mlalakuwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mwenzao.
Hii si mara ya kwanza kwa biskuti za aina hiyo kukamatwa katika mazingira yanayowahusisha vijana hasa wanafunzi wa vyuo, hali inayoashiria kengele ya hatari kwa kundi hilo.
Akizungumzia hilo Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema vijana hao walikutwa na biskuti 140 za bangi, puli nane, na paketi tisa za bangi zenye jumla ya kilo 2.858.
“Hii inaonesha namna vijana wetu wanavyohatarisha maisha yao kwa kujihusisha na utengenezaji wa bidhaa zenye dawa za kulevya kwa ajili ya starehe,”amesema Lyimo,
Kufuatia hilo amewaonya wanafunzi wa vyuo vikuu kuacha mara moja kujihusisha na dawa za kulevya na badala yake kutumia muda wao katika masomo ili kutimiza ndoto zao.
Chanzo: Mwananchi