Wakati Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) ikieleza sababu za baadhi ya kampuni kusitisha safari zake kati ya kesho Jumanne Oktoba 28-30, 2025, Chama cha Kutetea Abiria kimeeleza sababu hizo hazina mashiko kwani kila mtu ana shida zake za kijamii na kifamilia.
Baadhi ya kampuni za usafirishaji wa barabara na nyingine za majini zimetangaza kusitisha safari zake kati ya kesho Oktoba 28, hadi 29 na nyingine kwenda hadi Oktoba 30 ili kupisha shughuli ya upigaji kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyia Oktoba 29, 2025.
Baadhi ya kampuni za mabasi yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, Tarime (Mara), Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Mpanda (Katavi), Bukoba, Karagwe (Kagera), Kigoma na baadhi ya mikoa imetangaza kutosafirisha abiria Oktoba 29, siku ambayo Watanzania watapiga kura.
Kampuni ya Azam Marine na Zan Fast Ferries nazo zimetoa taarifa kwa umma kwamba Oktoba 29, 2025 hazitatoa huduma ya usafiri majini iwe Dar es Salaam-Zanzibar au Zanzibar- Dar es Salaam hadi Oktoba 30.
Hata kwenye mitandao yao, ukitaka kukaa tiketi tarehe hiyo haikupi nafasi ya kuichagua.
Chanzo: Mwananchi