Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Wahamiaji Haramu 11 Toka Bangladesh Wanaswa Morogoro

Wahamiaji haramu 11 kutoka mataifa ya Bangladesh, Somalia, Ethiopia na Burundi wamekamatwa na Ofisi ya Uhamiaji mkoani Morogoro, wakidaiwa kuingia nchini kinyume cha sheria na kujificha katika pori lililopo kitongoji cha Ranchi Dakawa, wilayani Mvomero.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Morogoro, Saada Nantepe, alisema watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia taarifa zilizotolewa na raia wema, ambapo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama waliweza kuwabaini na kuwakamata.

Nantepe alisema kuwa uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini njia walizotumia kuingia nchini pamoja na mtandao unaohusika na usafirishaji wa wahamiaji haramu.

Ametaja waliokamatwa kuwa ni raia wa Bangladesh: Miraz Husein (21), Arif Rahman (18), Azad Hosein (31), Maniki (25), Seif Islam (29), na Mohamed Ripuni (41).

Wengine ni raia wawili wa Somalia, Amnaj Ahmed (18) na Abdullah Bilod (18), huku raia wa Ethiopia wakiwa Yerekigi Merise (20) na Fahomumu Skoma (18), pamoja na raia mmoja wa Burundi mwenye umri wa miaka 24.

“Idara ya Uhamiaji inatoa wito kwa raia wote wa kigeni kuingia nchini kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Vilevile tunawaomba raia wema waendelee kutoa taarifa kuhusu wageni wanaoingia nchini bila kibali ili hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema Nantepe.

Baadhi ya wananchi wa Morogoro wamepongeza hatua hiyo, wakisema inaonyesha utendaji thabiti wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kulinda mipaka ya nchi.

Mmoja wa wananchi hao, Joyce James, alisema Serikali imeonyesha kujali usalama wa taifa kwa kuendelea kudhibiti wageni wanaoingia kiholela, akisisitiza kuwa baadhi yao huingia kwa nia mbaya na kutishia amani ya nchi.

Kwa upande wake, Fatma Rajabu alisema anashangazwa na kukamatwa kwa wahamiaji haramu katika mkoa wa Morogoro ambao si wa mpakani, akitoa wito kwa vyombo vya ulinzi vinavyosimamia mipaka kufanya kazi kwa umakini zaidi, huku wananchi wakiendelea kutoa ushirikiano ili kuzuia wageni kuingia kiholela nchini.

 

Chanzo: Nipashe

Kuhusiana na mada hii: