Serikali ya Zanzibar imetangaza mpango wa kuanza kununua mchanga kutoka Tanzania Bara kwa ajili ya kutumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa visiwani humo.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Nadir Abdul Latif, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya siku 100 za uongozi wa Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, katika kipindi cha pili cha uongozi wake.
Waziri Nadir amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na Zanzibar kukabiliwa na uhaba wa rasilimali ya mchanga unaoweza kukidhi mahitaji makubwa ya ujenzi, hasa katika kipindi hiki ambacho serikali inaendelea kutekeleza miradi mingi mikubwa ya maendeleo.
Amefafanua kuwa mchanga utakaoagizwa kutoka Tanzania Bara utatumika mahsusi katika miradi mikubwa ya ujenzi inayotekelezwa na serikali pamoja na ile inayohusisha uwekezaji mkubwa, ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo haukwami kutokana na changamoto ya upatikanaji wa mchanga.
“Tumegundua kuwa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa Zanzibar kwa sasa inahitaji kiasi kikubwa sana cha mchanga. Kutokana na hali hiyo, serikali imefanya tathmini na kuona ni vyema kuanza kuagiza mchanga kutoka Tanzania Bara kwa ajili ya miradi hiyo mikubwa,” amesema.
Ameongeza kuwa hatua hiyo pia inalenga kulinda mazingira ya Zanzibar kwa kupunguza uchimbaji mkubwa wa mchanga ndani ya visiwa hivyo ambao unaweza kusababisha athari za kimazingira ikiwemo uharibifu wa ardhi, mmomonyoko wa udongo na kuathiri mifumo ya ikolojia.
Hata hivyo, Waziri huyo amesisitiza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaohitaji mchanga kwa ajili ya shughuli ndogo za ujenzi kama ujenzi wa nyumba binafsi au utengenezaji wa matofali, hawatalazimika kununua mchanga kutoka Tanzania Bara.
Chanzo; Nipashe