Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu imetoa hukumu ya kihistoria leo Ijumaa, Machi 6, 2026, kwa kuitupilia mbali kesi iliyokuwa ikipinga uhalali wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020.
Mahakama hiyo iliyopo jijini Arusha imesema kuwa madai ya walalamikaji hayakuwa na uzito wa kisheria wala ushahidi wa kutosha kuthibitisha ukiukwaji wa misingi ya kidemokrasia.
Uamuzi huo unahitimisha shauri lililoanza Novemba 2020, likiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, kabla ya kuridhiwa kuendelezwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, kufuatia kifo cha Maalim Seif mwaka 2021.
Majaji wa Mahakama hiyo ya kikanda wamebaini kuwa, licha ya malalamiko mazito yaliyowasilishwa na wadai akiwemo Ado Shaibu, wagombea wawili na wapiga kura watatu hapakuwa na ushahidi wa kuaminika wa kuziunganisha tuhuma hizo na ukiukwaji wa sheria za uchaguzi.
Walalamikaji walikuwa wakidai kuwepo kwa matumizi ya nguvu, ukiukwaji wa haki za kisiasa na haja ya kufanya mageuzi ya Katiba na sheria za uchaguzi.
Chanzo; Eatv