Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Basi Lakamatwa na Tani 9 Dawa za Kulevya, Shamba Lateketezwa

Katika miezi ya Januari na Februari 2026, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata tani 9.93 za dawa za kulevya za aina mbalimbali, chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuteketeza ekari 87.5 za mashamba ya bangi.

Katika operesheni hizo, magari sita na pikipiki 29 vilikamatwa, huku jumla ya watuhumiwa 151 wakitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu huo.

Kwa kushirikiana na maafisa wa Forodha wa Mutukula, mamlaka hiyo ilikamata boksi 105 za Pethidine (chupa 1,045), boksi 31 za Morphine Sulphate (chupa 310) na boksi 44 za Fentanyl (chupa 440).

Dawa hizo zilikutwa katika basi la kampuni ya SR Classic lenye namba za usajili 5673AB04, likifanya safari kati ya Uganda, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakati wa ukaguzi katika kituo cha forodha cha Mutukula.

Dawa aina ya Pethidine, Morphine na Fentanyl ni dawa za kundi la afyuni (opioids) zinazotumika hospitalini kupunguza maumivu makali, lakini zikichepushwa hutumika kama dawa za kulevya na kusababisha uraibu na vifo kutokana na athari zake katika moyo, mfumo wa fahamu na upumuaji.

Kwa mujibu wa sheria za nchini, dawa hizo zimedhibitiwa chini ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, na Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, ambapo uingizaji na usambazaji wa dawa za nakotiki unaruhusiwa kufanywa na MSD pekee.

Katika operesheni nyingine, bangi aina ya skanka imekamatwa kwa wingi jijini Dar es Salaam, Mbeya, Arusha na mikoa mingine.

Dar es Salaam, mtuhumiwa mmoja alikamatwa na kilogramu 81.883 za skanka zilizokuwa zimefichwa ndani ya lori lililobeba matunda. Chanika Buyuni, watuhumiwa wawili walinaswa na kilogramu 488.64 za skanka.

Mbeya, watuhumiwa sita walikamatwa katika matukio tofauti wakisafirisha jumla ya zaidi ya kilogramu 76 za skanka. Arusha, watuhumiwa wawili walikamatwa na kilogramu 363.45 za mirungi.

Aidha, katika operesheni zilizofanyika mikoa mbalimbali ikiwemo Tabora, Tanga, Mwanza, Shinyanga, Katavi, Mtwara, Mara, Morogoro, Kigoma, Ruvuma na Kilimanjaro, zilikamatwa tani 5.24 za bangi, tani 4.04 za mirungi na gramu 72 za heroin.

 

Chanzo; Global Publishers

Kuhusiana na mada hii: