Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Bei ya Bidhaa Kilio Tanzania

Baada ya ukimya uliosababishwa na maandamano yaliyodumu kwa siku nne, shughuli za kijamii na kiuchumi zimeanza kurejea nchini Tanzania. Waandishi habari walioko katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Songwe wameiambai BBC kuwa maduka, masoko, na huduma mbalimbali zimeanza kutengamaa ingawa athari za maandamano bado zinaonekana.

Maandamano hayo, ambayo yalianza siku ya uchaguzi, yamesababisha vifo na majeruhi kadhaa pamoja na uharibifu mkubwa wa mali hasa za umma na binafsi za watu wanaohusishwa na utawala. Licha ya shughuli kurejea taratibu, ghasia hizo zimepelekea ongezeko la bei za bidhaa muhimu katika baadhi ya maeneo ya nchi.

"Ukiangalia nyama, nyama sasa hivi kilo shilingi 15,000 au 20,000. Mimi kama mama lishe mdogo napika kilo zangu mbili au tatu, hiyo nyama nainunua kilo ngapi?" anauliza Mama Dulla, mmoja wa wajasiriamali wadogo wauza chakula maarufu kama mama ntilie jijini Dar es Salaam.

"Unga tuliokuwa tunanunua shilingi 1,600 sasa hivi unga ni shilingi 2,000 mpaka 2,200, je sisi mama lishe sahani ya chakula tutauza shilingi ngapi, hapo ndipo changamoto," anaongeza mfanyabiashara huyo akieleza kuwa tangu Oktoba 29, 2025 hajarejea kazini, jambo lililosababisha apoteze wateja na kutumia mtaji wake kwa matumizi ya nyumbani.

Mama Dulla anasema ingawa serikali imetangaza kurejea kwa shughuli za kawaida, hana mtaji wa kuanza upya. "Tangazo limetoka, fanyeni shughuli zenu, je huo msingi upo? Sasa naanza kutafuta msingi mpya, ambao ni changamoto, sijui nitaanza lini tena biashara," anasema.

Maria, mfanyabiashara mwingine jijini humo, anakumbana na changamoto kama hizo. "Sijaweza kutoka kwa sababu ya mazingira jinsi yalivyo, ili niweze kufika sehemu yangu ya kazi nahitaji usafiri. Daladala chache zinafanya masafa, na sio kila sehemu zinafika, bajaji wanataka nauli kubwa, mimi siwezi kumudu," anasema huku akitoa wito kwa serikali "iangalie upande wa bidhaa kupanda kwa bei kuwe afadhali kwa sisi wajasiriamali wadogo pia tuweze kuendesha maisha yetu."

Akiapishwa mwishoni mwa wiki, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kurejea kwa hali ya kawaida nchini.

"Kamati ya ulinzi na usalama ya kitaifa, na kamati za ulinzi za mikoa na wilaya, nawataka muhakikishe kuanzia leo maisha ya wananchi yanarejea mara moja," alisema.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu idadi kamili ya vifo, majeruhi au uharibifu uliosababishwa na maandamano hayo, ambayo wachambuzi wanasema ni makubwa zaidi kushuhudiwa nchini humo tangu ilipopata uhuru mwaka 1961.

Waangalizi wa masuala ya kisiasa wanasema maandamano hayo yamechochewa na madai ya kutoridhika na mfumo wa uchaguzi, ukosefu wa uhuru wa kisiasa, pamoja na madai ya kudorora kwa demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari. Madai ambayo mara kadhaa Serikali imeyapinga, ikisema imeyashughulikia kwa kiwango chake ikiwemo kutengenezwa kwa sheria mpya ikiwemo iliyoanzisha Tume Huru ya Uchaguzi, na kurekebisha maeneo mengi yaliyokuwa yakilalamikiwa.

Katika uchaguzi wa Oktoba 29, Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania (INEC) ilimtangaza Rais Samia Suluhu Hassan mshindi wa urais kwa asilimia 98 ya kura, ikimpa nafasi ya kuendelea kuongoza kwa muhula wa pili wa miaka mitano. Rais Samia alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Pombe Magufuli.

Maandamano hayo yalianza siku ya uchaguzi Jumatano iliyopita, ambapo baadhi ya waandamanaji walichana mabango ya Rais Samia na kuchoma majengo ya serikali. Polisi na vyombo vingine vya dola vilitumika kukabiliana na waandamanaji. Wengi wa waandamanaji walikuwa wakilalamikia kutoshiriki kwa wagombea wawili wakuu wa upinzani, Tundu Lissu na Luhaga Mpina.

Lissu na chama chake cha CHADEMA, chama kikuu cha upinzani kilijiondoa katika kinyang'anyiro hicho, kikidai kufanyika kwa mabadiliko ya sheria za uchaguzi kabla ya uchaguzi mwingine wowote, huku Mpina wa ACT Wazalendo aliondolewa na INEC kwa madai ya kutokidhi vigezo vya kisheria.

 

Chanzo; Bbc

Kuhusiana na mada hii: