Serikali nchini Tanzania inakabiliwa na shinikizo linaloongezeka kufuatia mauaji yaliyoshuhudiwa wakati na baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita, huku chama kikubwa zaidi cha upinzani CHADEMA kikivishutumu vikosi vya usalama kuhusika na vitendo hivyo pamoja na kuitupa au kuizika kwa siri miili ya mamia ya watu waliouawa katika ghasia zilizoushtua ulimwengu.
Maandamano ya kupinga uchaguzi wa Oktoba 29 yalishuhudiwa kwa siku kadhaa katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania huku vijana wakiingia mitaani katika miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na mahali pengine ili kupinga kile walichotaja kwamba halikuwa zoezi la huru wala haki.
Vikosi vya usalama vilijaribu kuyazima maandamano hayo kwa kutumia mabomu ya machozi na hata kuwafyatulia waandamanaji risasi za moto huku amri ya kutotoka nje usiku ikitangazwa nchini humo. Brenda Rupia, mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa chama cha upinzani Chadema ameliambia shirika la habari la AP kwa njia ya simu kuwa kwa sasa mioyo ya Watanzania inavuja damu na kwamba hili ni jambo jipya kwao.
Chanzo; Dw