Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa kuhusu kuwepo kwa kimbunga kinachoitwa “CHENGE” katika Bahari ya Hindi, kaskazini mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar, takribani kilomita 2,400 kutoka mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Kwa mujibu wa TMA, kimbunga hicho kilianza kujitengeneza tarehe 17 Oktoba 2025 katika maeneo ya mashariki mwa Bahari ya Hindi na kimeendelea kuimarika. Uchambuzi wa hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha siku nne hadi tano zijazo — kati ya tarehe 26 na 27 Oktoba 2025 — kimbunga “CHENGE” kinatarajiwa kusogea kuelekea magharibi mwa Bahari ya Hindi, katika ukanda wa pwani ya Tanzania, ingawa kitakuwa kikipungua nguvu yake
TMA imesisitiza kuwa inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho pamoja na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa nchini, na itatoa taarifa zaidi pale inapobidi.
TMA imewataka watumiaji wa bahari pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa kutoka TMA, sambamba na kupata ushauri na miongozo kutoka kwa wataalam wa sekta husika.
Chanzo: Wasafi