Asilimia kubwa ya wananchi waliolipwa fidia ya makaburi ya Bongololo yaliyopo Mtaa wa Shimo la Udongo, Kata ya Kurasini, kwa ajili ya kupisha ujenzi wa bandari kavu, wamekacha kwenda kuzika.
Kazi hiyo ya uhamishaji imeanza leo Jumatatu, Desemba 29, 2025, baada ya kumalizika kwa ulipaji wa fidia iliyofanyika kwa takribani wiki mbili.
Katika ulipaji fidia huo, kila kaburi mtu alilipwa Sh300,000 kama rambirambi huku gharama za kuyahamisha, ikiwemo majeneza, sanda na watu wanaofukua, zikigharamiwa na mwekezaji.
Kazi hiyo itaendelea kwa siku nane, ambapo makaburi zaidi ya 2,800 yameutambuliwa, huku mabaki ya miili yakihamishiwa katika makaburi ya Halmashauri ya Sako yaliyopo Mbagala jijini humo.
Akizungumza na Mwananchi, Mwakilishi wa mwekezaji wa bandari hiyo, Mohammed Kamilagasa, amesema katika kazi ya leo ya kuanza kuhamisha waliwapigia simu watu 500, lakini waliojitokeza kwenda kushiriki ni watu 12 pekee.
“Hii inasikitisha sana kwa kuwa ibada ya kuzika ilikuwa ni muhimu kuliko tukio la kuchukua hela, lakini ndivyo ilivyo,” amesema Kamilagasa.
Chanzo; Mwananchi