Familia ya mgombea ubunge kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Jimbo la Siha, Daudi Ntuyehabi aliyeuawa na wananchi wenye hasira kali, imeeleza majonzi makubwa kufuatia kifo cha ndugu yao huyo.
Mgombea huyo alishambuliwa na kundi la watu zaidi ya wanane baada ya kudaiwa kumchoma kisu kijana mmoja wakati alipokwenda kuamua ugomvi uliotokea katika ‘grocery’ ya vinywaji.
Familia hiyo imeiomba Serikali kuingilia kati na kuhakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
Dada wa marehemu, Annet Ntuyehabi, amesema kifo hicho kimekatisha ndoto za ndugu yao aliyekuwa na malengo ya kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Siha kupitia nafasi ya ubunge.
Amesema pia kuwa marehemu ameacha watoto wawili — mmoja wa darasa la nne na mwingine wa darasa la kwanza — jambo linaloongeza majonzi kwa familia.
Shemeji wa marehemu, Rogate Mwandry, amesema familia imeliweka suala hilo mikononi mwa Serikali na vyombo vya usalama, huku Alpha Mwandry, naye akieleza kuwa wanasubiri ndugu kutoka Geita kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.
Kwa sasa, watu wanane wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi na kusababisha kifo cha mgombea huyo wa ubunge.
Chanzo: Global Publishers