Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ameutaka uongozi wa Wizara ya Afya ufuatilie suala la upatikanaji wa dawa mahsusi hospitalini ili kuondoa dosari ndogondogo zilizopo
Ametoa wito huo leo Jumamosi, Desemba 20, 2025 wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Lindi na viongozi wa sekta ya afya mara baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi inayojengwa katika eneo la Mitwero, nje kidogo ya mji wa Lindi.
“Kitengo chenu cha utafiti kifanye kazi kubaini ni aina gani ya dawa zinahitajika hapa mkoani Lindi. Bohari ya Dawa ifuatilie vizuri na kuleta dawa zinazotakiwa,” amesema wakati akimwagiza Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi ambaye alikuwepo katika ziara hiyo.
Amesema usipofanyika utafiti huo, Bohari ya Dawa watajikuta wanapeleka dawa nyingi mahali ambako hazihitajiki. “Unaweza kujikuta unapeleka dawa nyingi za malaria huko Zanzibar wakati wao hilo tatizo hawana kabisa,” amesema.
Chanzo; Eatv