Dar es Salaam, Tanzania, 6 Agosti 2026: Katika hatua muhimu kwa maendeleo ya mchezo wa kuendesha baiskeli nchini Tanzania, Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA), leo imetangaza rasmi kubadilishwa kwa jina la msafara wa baiskeli wa Twende Butiama na kuwa Nyerere Cycling Tour, huku pia wakitangaza kuzindua mashindano mapya ya mbio za baiskeli za kilomita 109 za Vodacom Coastal Classic, zinazolenga kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya mashindano ya baiskeli.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, msafara huu umekuwa ukienzi urithi wa kudumu wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa kuendeleza fursa sawa kwa wote kupitia uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia, ujenzi wa miundombinu ya vyoo, pamoja na kuchangia vifaa vya kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kila mtoto aweze kupata fursa ya elimu.
Hadi sasa, msafara huo umefikia zaidi ya shule 107 na kuboresha maisha ya wanafunzi zaidi ya 75,000 wanaofaidika kupitia ujenzi wa madarasa bora na jumuishi yanayokidhi mahitaji ya wanafunzi wote.

Vodacom Tanzania Foundation ilianza kushirikiana na CHABATA kufadhili msafara huu miaka mine iliyopita, na katika kipindi hicho msafara wa Twende Butiama umekuwa mara nne zaidi, huku ukivutia washiriki kutoka Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa. Msafara wa mwaka huu utafanyika kuanzia tarehe 5 hadi 14 Oktoba 2026, washiriki wakianzia Bagamoyo hadi Butiama.