Dahane Beida kutoka Mauritania ametajwa kuwa mwamuzi wa kati katika mechi ya Kundi C ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) kati ya Nigeria na Tanzania, kwa mujibu wa shirikisho la soka Afrika (CAF).
Beida anayetajwa kuwa miongoni mwa waamuzi wenye uzoefu mkubwa barani Afrika kwa sasa, katika mechi ya ufunguzi ya AFCON 2025 iliochezwa jana Jumapili, Desemba 21 kati ya wenyeji Morocco na Comoros, alikuwa sehemu ya waamuzi wa Teknolojia ya Video ya Mwamuzi Msaidizi (VAR).
Katika mechi hiyo ya ufunguzi, Morocco waliibuka na ushindi wa mabao 2–0 dhidi ya Comoros, mabao yaliyofungwa na Brahim Díaz na Ayoub El Kaabi, na hivyo kuanza mashindano hayo kwa kishindo.
Timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, itaanza kampeni yake ya Kundi C dhidi ya Tanzania kesho Jumanne, katika Uwanja wa Complexe Sportif de Fès. Mechi hiyo itakuwa ni mara ya pili kwa mataifa hayo mawili kukutana katika historia ya mashindano ya AFCON.
Mara ya kwanza Nigeria na Tanzania zilipokutana ilikuwa katika fainali za AFCON 1980, ambapo Nigeria iliibuka na ushindi wa mabao 3–1.
Chanzo; Mwanaspoti