Nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry, ameweka historia mpya baada ya kumvua LeBron James taji la mchezaji anayelipwa zaidi katika ligi ya mpira wa kikapu ya NBA, na hivyo kumaliza utawala wa miaka 11 wa James kwenye orodha hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Forbes, Curry anatarajiwa kupata jumla ya dola milioni 159.6 (sawa na zaidi ya shilingi bilioni 420 za Kitanzania) msimu huu kiasi kinachojumuisha mshahara wake kutoka Warriors pamoja na mapato ya mikataba ya nje ya uwanja, ikiwemo ushirikiano wake mkubwa kupitia Curry Brand chini ya kampuni ya Under Armour.
Kiasi hicho kinampita LeBron James wa Los Angeles Lakers, ambaye atavuna takribani dola milioni 137.6 msimu huu. Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha misimu 17 ya Curry kushika nafasi ya kwanza kwenye orodha ya kila mwaka ya Forbes.
Kwa ujumla, wachezaji 10 wanaoongoza kwa malipo katika NBA wanatarajiwa kupata jumla ya dola milioni 902 msimu huu rekodi mpya inayochochewa na mapato makubwa ya ligi na mkataba mpya wa haki za matangazo wenye thamani ya dola bilioni 76, ambao unatarajiwa kuendelea kupandisha mishahara ya wachezaji kwa miaka ijayo.
Chanzo: Bongo 5