Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Bloomberg, Cristiano Ronaldo amefanikisha historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza wa soka duniani kufanikisha hadhi ya bilionea, akiwa na utajiri unaokadiriwa kufikia dola bilioni 1.4 za Kimarekani.
Ronaldo amejumuishwa kwenye Bloomberg Billionaires Index, orodha ya watu matajiri zaidi duniani, jambo ambalo ni la kipekee kwa mchezaji wa soka. Chanzo kikuu cha utajiri huu ni mkataba wake wa kifahari na klabu ya Al Nassr ya Saudi Arabia, unaomlipa zaidi ya dola milioni 200 kwa mwaka, ukijumuisha bonasi, malipo yasiyo ya kodi, na mikataba ya matangazo.
Zaidi ya uwanja wa soka, Ronaldo amejijengea ufalme wa kibiashara kupitia brand yake ya CR7, inayojumuisha mavazi, hoteli, manukato, na bidhaa za fitness, jambo lililoongeza mapato yake hadi kiwango kisichowahi kufikiwa na mchezaji mwingine wa soka.
Wataalamu wa uchumi wa michezo wanasema mafanikio haya yanaonyesha jinsi Ronaldo alivyochukua soka zaidi ya mchezo na kuugeuza kuwa biashara ya kimataifa. Kila mchezo, kila tangazo, na kila bidhaa anayoitoa inaongeza thamani ya jina lake duniani kote.
Kwa sasa, Bloomberg inakadiria Ronaldo kuwa na utajiri mkubwa kuliko mastaa kama Lionel Messi, LeBron James, na Tiger Woods, lakini yeye ndiye wa kwanza kutajwa rasmi kama bilionea wa soka, akithibitisha kuwa ni GOAT wa biashara ya soka.
Chanzo: Global Publishers