GWIJI wa soka nchini England, Alan Shearer, amemshambulia nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, akimweleza kuwa amefanya kitendo cha “kusikitisha” katika tukio lililosababisha Phil Foden kutolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa Manchester Derby wikiendi iliyopita.
Foden alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 23 baada ya kumrushia mguu Fernandes, na kuiacha Manchester City ikicheza pungufu kwa sehemu kubwa ya mchezo wa Jumapili ambao mwisho City ilishinda bao 1-0.
Hata hivyo, Shearer anaamini Fernandes alichangia kwa kiasi kikubwa tukio hilo, baada ya kuonekana kumpiga Foden akiwa amelala chini, kabla ya kiungo huyo wa Manchester United kuanguka na kujizungusha uwanjani akionyesha maumivu.
Shearer ambaye ni mchezaji wa zamani wa Newacastle amesisitiza kuwa mwamuzi Michael Oliver alipaswa kutoa adhabu sawa kwa wachezaji hao wawili.