Mashindano ya Kilombero Golf Open 2026 yameanza rasmi leo katika uwanja wa gofu wa Kilombero, huku wapenzi wa mchezo huo wakijiandaa kushuhudia siku tatu za ushindani, umahiri na uchezaji wenye kuzingatia misingi ya uanamichezo.
Mashindano hayo ya siku tatu, ambayo yanafanyika kwa mara ya kwanza katika viwanja vya gofu vya Kilombero Sugar, yamevutia wachezaji kutoka vilabu mbalimbali vya gofu nchini. Lengo la mashindano hayo ni kuendeleza mchezo wa gofu, kuimarisha ushindani miongoni mwa wachezaji na kuhamasisha ushiriki mpana wa wadau katika maendeleo ya mchezo huo nchini Tanzania.

Mashindano ya mwaka huu yamezikutanisha timu saba kutoka vilabu vya gofu nchini, ambavyo ni TPDF Lugalo Golf Club, Dar es Salaam Gymkhana Club, Kilimanjaro Golf Club, TPC Club, Morogoro Gymkhana Club, Mufindi Golf Club na Kilombero Golf Club. Ushiriki wa timu hizo unatoa fursa kwa wachezaji kushindana, kujenga mahusiano na kubadilishana uzoefu, huku wakichangia ukuaji wa mchezo wa gofu nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Pierre Redinger, Mwenyekiti wa Kilombero Country Club na Mkurugenzi wa wakulima Kilombero Sugar amesema kuwa kuandaa mashindano hayo ni fursa muhimu ya kuwakutanisha wachezaji kutoka vilabu mbalimbali, kuimarisha ushindani wa kimichezo na kuhamasisha watu wengi zaidi kushiriki katika mchezo wa gofu.
“Kuandaa mashindano ya Kilombero Golf Open kunatupa fursa ya kuwakutanisha wachezaji wa gofu kutoka vilabu mbalimbali, kuimarisha ushindani na kuhamasisha watu wengi zaidi kuufahamu na kushiriki katika mchezo huu. Tunaamini mashindano haya yatachangia maendeleo endelevu ya gofu na kuongeza ushiriki wa wachezaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.”

Benki ya NBC, ambayo ni mdhamini wa mashindano hayo, ilieleza kuwa ushirikiano wake na Kilombero Sugar unalenga kusaidia maendeleo ya mchezo wa gofu, kuwawezesha vijana kutambua na kukuza vipaji vyao, pamoja na kutengeneza fursa kwa wachezaji kupata kutambulika katika majukwaa ya kimataifa.
Jimmy Myalize, Mkuu wa Huduma za Miamala na Amana za Wateja Wakubwa katika Benki ya NBC, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuendeleza michezo na kukuza vipaji vipya.
“Udhamini wetu wa mashindano ya Kilombero Golf Open 2026 unaonesha umuhimu wa ushirikiano katika kuendeleza michezo na kutengeneza fursa kwa vijana. Kupitia ushirikiano wetu na Kilombero Sugar pamoja na wadau wengine, tunalenga kuchangia mazingira yatakayowezesha vipaji vipya kutambuliwa, kukuzwa na kupewa fursa za kushiriki katika mashindano mbalimbali.”
Kwa upande wao, Isiaaka Dunia na Vicky Elias, wachezaji wa gofu kutoka TPDF Lugalo Golf Club jijini Dar es Salaam, wamewahimiza vijana kujitokeza kushiriki katika mchezo huo na kutumia fursa zinazotokana na gofu. Pia, waliwataka wazazi na walezi, hususan akina mama, kuwahamasisha mabinti zao kushiriki katika mchezo huo, kukuza uwezo wao na kufuatilia malengo yao ya kimichezo.
“Tunawahimiza vijana wengi zaidi kuanza kucheza gofu ili waweze kutambua na kukuza vipaji vyao. Wazazi pia wana jukumu muhimu la kuwasaidia watoto wao, wakiwemo wasichana, na kuwapa fursa ya kushiriki katika michezo ili kukuza uwezo wao,” alisema Isiaaka Dunia, mchezaji wa gofu kutoka TPDF Lugalo Golf Club.

“Tungependa kuona wasichana wengi zaidi wakishiriki katika mchezo wa gofu. Wazazi na walezi wana jukumu muhimu la kuwahamasisha mabinti zao kushiriki katika michezo na kuwaunga mkono ili waweze kutumia fursa zilizopo kukuza vipaji vyao,” alisema Vicky Elias, mchezaji wa gofu kutoka TPDF Lugalo Golf Club.
Mashindano ya Kilombero Golf Open 2026 yanatarajiwa kuhitimishwa Jumapili, tarehe 11 Oktoba 2026, katika uwanja wa gofu wa Kilombero Sugar, Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro.