Wafanyabiashara nchini Tanzania sasa wanatarajiwa kunufaika na fursa mpya ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ununuzi wa magari ya biashara na mitambo, kufuatia ushirikiano kati ya Benki ya Exim Tanzania na Kampuni ya Six Continental Trading Company Limited.
Kupitia ushirikiano huo, wafanyabiashara wanaokidhi vigezo, ikiwemo biashara ndogo na za kati (SMEs) pamoja na makampuni mbalimbali, watapata ufadhili wa hadi asilimia 80 ya gharama ya ununuzi wa magari mapya ya biashara, malori na mitambo mizito, huku wakichangia asilimia 20 pekee ya thamani ya mali husika.

Mpango huo pia unatoa masharti nafuu ya urejeshaji wa mkopo kwa kipindi cha hadi miaka mitano, ambapo riba itahesabiwa kwa mfumo wa salio linalopungua na viwango vyake vikijadiliwa kulingana na mahitaji ya mteja.
Sekta mbalimbali muhimu za uchumi, ikiwemo usafirishaji na ugavi, ujenzi, kilimo pamoja na uzalishaji, zinatarajiwa kunufaika na huduma hiyo ambayo inahakikisha malipo yanafanywa moja kwa moja kwa wasambazaji mara baada ya mkopo kuidhinishwa. Hatua hiyo itaziwezesha biashara kupata vifaa na zana muhimu bila kuathiri mtaji unaotumika katika shughuli za kila siku.

Kwa kupunguza mzigo wa mtaji wa awali, ushirikiano huo unalenga kusaidia biashara kuongeza uwezo wa uzalishaji na utoaji huduma, kuimarisha mifumo ya usambazaji na kufungua fursa mpya za ukuaji katika soko la ndani na la kikanda.
Mbali na ufadhili huo, kifurushi cha huduma kinajumuisha bima ya magari pamoja na bima ya mkopo (Credit Life Insurance), hatua inayolenga kutoa ulinzi zaidi kwa wateja katika kipindi chote cha marejesho.
Benki ya Exim Tanzania na Six Continental Trading Company Limited zimesema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kuwezesha biashara kupata magari mapya ya kibiashara, kupanua shughuli zao za usafirishaji na kuongeza uwezo wa kuhudumia masoko yanayokua kwa kasi nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki.