Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

VISIONFUND TANZANIA MICROFINANCE BANK (VFT) YAZINDUA RASMI  “SMART BANKING”

VisionFund Tanzania Microfinance Bank Limited (VFT) imezindua rasmi huduma yake ya benki kidijitali, VFT Smart Banking App, hatua inayolenga kusogeza huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi, kupunguza gharama na muda wa kupata huduma, na kuongeza fursa za ushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Kupitia VFT Smart Banking App, wateja wanaweza kupata huduma mbalimbali za kifedha moja kwa moja kupitia simu zao za mkononi, bila kulazimika kutembelea tawi kwa kila huduma.

Huduma kuu zinazotolewa kupitia VFT Smart Banking App ni:

1.     Fungua Akaunti Papo Hapo — wakati wowote na mahali popote Kupitia Simu ya Mkononi

2.     Kopa hadi Mara Tatu ya Akiba Yako — bila dhamana, kupitia Dunduliza Group Account

3.     Lipa Bila Makato — lipa bili, tozo za Serikali na Lipa Namba Bila Gharama ya Muamala.

 Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa VisionFund Tanzania Microfinance Bank Limited, Bw. Rogathe Godson, alisema VFT Smart Banking ni ubunifu unaotumia teknolojia kushughulikia changamoto halisi zinazokwamisha upatikanaji na matumizi ya huduma za kifedha, hususan kwa wajasiriamali wadogo, wafanya biashara zisizo rasmi, na wananchi wanaoishi mbali na vituo vya huduma za kifedha.

“Alisema changamoto ya kwanza ni ukosefu wa dhamana kwa wananchi wanaohitaji mikopo.

“Wananchi wengi, hususan wajasiriamali wadogo na watu wenye shughuli za kiuchumi zisizo rasmi, wanaweza kuwa na uwezo wa kuweka akiba na kurejesha mkopo, lakini hawana mali zinazoweza kutumika kama dhamana.

Kupitia VFT Smart Banking “Dunduliza Group Account inajibu changamoto hii kwa kutumia mpango wa mteja wa kuweka akiba kama msingi wa kumwezesha mwanachama kupata mkopo. Kupitia Dunduliza, mwanachama anaweza kukopa hadi mara tatu ya akiba yake bila dhamana, kwa kuzingatia vigezo na masharti ya huduma.

“Hii inabadilisha namna tunavyofikiria kuhusu uwezo wa mteja kukopa — kutoka kutegemea mali alizonazo kama dhamana pekee, kwenda pia kuangalia nidhamu yake ya kuweka akiba (savings plan) kama sehemu ya msingi wa kupata mkopo.”

Aliongeza kuwa changamoto ya pili ni gharama za miamala, ambazo zinaweza kuwa kikwazo kwa wananchi kutumia njia za kidijitali.

“VFT Smart Banking inajibu changamoto hii kwa kuwawezesha wateja kulipa bili, tozo za Serikali na Lipa Namba BURE bila gharama ya muamala.

 

“Tunaamini kuwa huduma za kidijitali zinapaswa kuwa na thamani halisi kwa mteja. Kupunguza gharama za miamala ni hatua muhimu katika kuhamasisha wananchi wengi zaidi watumie njia za kidijitali na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.”

Kwa mujibu wa Bw. Godson, changamoto ya tatu ni gharama ya kumhudumia mteja aliye mbali na tawi.

“Kumhudumia mteja katika maeneo yaliyo mbali, hususan maeneo ya vijijini, kunahitaji uwekezaji katika matawi, watumishi, miundombinu, usafiri na mifumo ya uendeshaji. Kadiri mteja anavyokuwa mbali na kituo cha huduma, ndivyo gharama na muda wa kumfikia unavyongezeka; na hii inasabisha aidha Huduma za kibenki zisifike vijijini au Huduma zifike kwa gharama kubwa sana ambapo Wateja wanashindwa kuzimudu.

“VFT Smart Banking inasaidia kukabiliana na changamoto hii kwa kumwezesha mteja kujihudumia kupitia simu yake ya mkononi. Mteja anaweza kufungua akaunti na kupata huduma mbalimbali za kifedha bila kulazimika kutembelea tawi.

“Hii inatusaidia kupunguza utegemezi wa miundombinu ya matawi kwa huduma zinazoweza kutolewa kidijitali, na hivyo kutengeneza fursa ya kuwafikia wateja wengi zaidi kwa ufanisi na gharama nafuu.”

Alisisitiza: “VFT Smart Banking siyo tu kuhusu kuweka huduma za benki kwenye simu. Ni kuhusu kutumia teknolojia kushughulikia changamoto za msingi zinazozuia upatikanaji na matumizi ya huduma za kifedha kwa wateja.”

 

 Mkurugenzi wa Uendeshaji wa VisionFund Tanzania Microfinance Bank Limited, Bw. Deogratius Siria, alisema mojawapo ya ubunifu muhimu katika VFT Smart Banking ni Dunduliza Group Account, ambayo inaunganisha utamaduni wa vikundi vya kuweka akiba (VICOBA) na uwezo wa benki pamoja na teknolojia ya kidijitali.

“VICOBA NA SACCOS zimeonyesha kwa muda mrefu kwamba wananchi wanaweza kuunganisha nguvu zao kupitia akiba na kusaidiana kupata fedha. Dunduliza Group Account inachukua msingi huo na kuuongezea nguvu ya benki na teknolojia, ili wanachama waweze kuweka akiba, kupata mikopo na kufuatilia shughuli zao za kifedha kwa njia salama na yenye uwazi zaidi.”

 

Kupitia Dunduliza Group Account, wanakikundi wanaweza kukopa hadi mara tatu ya akiba yao bila dhamana, kwa kuzingatia vigezo na masharti ya huduma.

Hivyo, tofauti na mfumo wa kawaida wa VICOBA ambapo fedha zinazokopeshwa hutokana zaidi na akiba ya wanachama, Dunduliza inaongeza nguvu ya kifedha ya benki ili kuwawezesha wanakikundi kupata mikopo inayozidi kiasi cha akiba walichoweka.

Kupitia Dunduliza, hadi theluthi moja ya wanachama wa kikundi wanaweza kupata mikopo kila mwezi, hata kama wanakikundi ni wengi sana mfano 300 ndani ya miezi mitatu wanakikundi wote wanaweza kuwa wameshachukua mikopo (mikopo kwa wanakikundi 100 kila mwezi; ambayo ndio theluthi moja)

Mfumo huu unatoa fursa kwa wanachama kupata fedha wanapozihitaji bila kutegemea utaratibu wa kusubiri zamu kama inavyoweza kutokea katika baadhi ya mifumo ya kawaida ya vikundi.

 

Dunduliza pia inatoa mikopo yenye muda wa marejesho wa hadi miezi mitatu, kwa gharama ya asilimia 4 kwa mwezi. Hii inawapa wanachama nafasi ya kupanga matumizi na marejesho ya mikopo yao kwa muda unaolingana na mahitaji yao na uwezo wao wa kifedha.

Mkurugenzi wa Fedha wa VisionFund Tanzania Microfinance Bank Limited, Bw. Henry Horombe, alisema kupunguza gharama za miamala ni hatua muhimu katika kuongeza matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali na kuchochea ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali.

“Uchumi wa kidijitali utakuwa na maana zaidi iwapo wananchi wa kawaida, hususan wale wenye kipato cha chini, wataweza kushiriki na kunufaika nao bila kukabiliwa na gharama zisizo za lazima.”

Alisema moja ya vikwazo vinavyoweza kuathiri matumizi ya huduma za malipo ya kidijitali ni gharama kubwa za miamala.

“Mteja anapotozwa ada kwa kila malipo, hususan katika miamala midogo au ya mara kwa mara, gharama hizo zinaweza kumkatisha tamaa kutumia njia za kidijitali na kumfanya aendelee kutegemea njia ya fedha taslimu.

“VFT Smart Banking inalenga kupunguza kikwazo hicho kwa kuwawezesha wateja kulipa bili, tozo za Serikali na Lipa Namba BURE bila ada ya muamala.

“Hii inafanya matumizi ya malipo ya kidijitali kuwa nafuu zaidi na inaweza kuwahamasisha wateja wengi zaidi kuhamia kwenye njia za kidijitali.”

Bw. Horombe alisisitiza kuwa lengo la VFT si kuweka huduma za benki kwenye simu pekee, bali kutumia teknolojia kuleta manufaa yanayoonekana katika maisha ya kila siku ya wateja.

“Tunapoondoa gharama kwenye huduma hizi, hatuondoi tu kikwazo kwa mteja mmoja mmoja, bali pia tunachangia kujenga mazingira wezeshi yanayohamasisha matumizi mapana zaidi ya malipo ya kidijitali katika shughuli za kila siku za wananchi na wafanya biashara.”

 

Kuhusiana na mada hii: