Waziri - Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, ameshiriki kikao maalum na Gavana wa Jimbo la Sverdlovsk, Denis Pasler, kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na uwezeshaji wa vijana.
Kikao hicho kilifanyika katika ofisi ya gavana huyo katika jiji la Ekaterinburg ikiwa ni pembezoni mwa Tamasha la Kimataifa la Vijana linaloendelea nchini Urusi, ambapo Jimbo la Sverdlovsk ni mwenyeji wa tamasha hilo linalowakutanisha vijana kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza katika kikao hicho, Gavana Pasler alieleza kuwa jimbo hilo limekuwa likitekeleza programu mbalimbali za elimu, utamaduni, michezo na kujitolea kwa lengo la kuwajengea vijana uzoefu na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na uchumi.
Kwa upande wake, Waziri Nanauka alitaka kufahamu sera na mikakati ambayo jimbo hilo limekuwa likitumia kukabiliana na ongezeko la idadi ya vijana, pamoja na namna vyuo vikuu vinavyowaandaa wanafunzi kuingia katika shughuli za kiuchumi baada ya kuhitimu.

Aidha, alihoji kuhusu uwepo wa programu za kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwasaidia kujiajiri ili kuongeza fursa za ajira na ubunifu.
Akijibu maswali hayo, Gavana Pasler alisema kuwa mipango yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Jimbo la Sverdlovsk imekuwa ikiwapa vijana kipaumbele. Alibainisha kuwa vyuo vikuu katika jimbo hilo vimeanzisha takribani programu saba maalum za elimu zinazolenga kuwaandaa vijana kwa soko la ajira na shughuli za uzalishaji.
Aliongeza kuwa wataalamu kutoka sekta mbalimbali wamekuwa wakishirikishwa kutoa mafunzo kwa vijana ili kuwajengea ujuzi unaohitajika katika mazingira ya sasa ya kiuchumi.
Gavana Pasler pia alisisitiza kuwa Jimbo la Sverdlovsk liko tayari kushirikiana na nchi mbalimbali katika kubadilishana uzoefu na mbinu bora za kuwawezesha vijana.

Akimhitimisha mazungumzo hayo, alimshukuru Waziri Nanauka pamoja na mawaziri wengine kutoka mataifa mbalimbali kwa kushiriki katika Tamasha la Kimataifa la Vijana, akieleza kuwa Ekaterinburg ipo tayari kuimarisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali yanayolenga maendeleo na ustawi wa vijana duniani.