Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Watanzania Walioshiriki Tamasha la Vijana Urusi Waeleza Waliyojifunza

Vijana waliowakilisha Tanzania katika Tamasha la Kimataifa la Vijana (International Festival of Youth – IFY 2026) lililofanyika jijini Ekaterinburg, Urusi, wamekutana na wenzao nchini kwa ajili ya kushiriki uzoefu na maarifa waliyoyapata wakati wa tamasha hilo lililowakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Mkutano huo ulifanyika katika Jumba la Urusi (Russian House) na kuhudhuriwa na vijana, maafisa kutoka Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Vijana.

Katika mkutano huo, wajumbe wa Tanzania walieleza kuwa ushiriki wao katika tamasha hilo uliwapa fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yakiwemo uongozi, biashara, ujasiriamali na diplomasia, sambamba na kujenga mitandao ya urafiki na ushirikiano na vijana kutoka takribani nchi 189 zilizoshiriki.

Vijana hao walitoa shukrani kwa Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi, Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania pamoja na Wizara ya Masuala ya Vijana ya Urusi kwa mchango wao katika kufanikisha ushiriki wa Tanzania kwenye tamasha hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sayansi na Utamaduni cha Urusi nchini Tanzania, Alexander Evstigneev, aliwapongeza vijana wa Tanzania kwa uwakilishi wao, akisema walichangia kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizotajwa na kujadiliwa zaidi wakati wa tamasha hilo.

Evstigneev pia aliahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi kupitia programu na matukio mbalimbali yanayolenga kuwawezesha vijana.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Urusi alisema taifa linajivunia kuona vijana wakitumia fursa za kimataifa kujifunza, kupata uzoefu mpya na kujenga mtandao wa mahusiano utakaowanufaisha wao binafsi na nchi kwa ujumla.

Alisema ushiriki wa vijana wa Tanzania nchini Urusi umeonyesha kuwa vijana wa taifa hilo wana uwezo wa kutimiza ndoto zao wanapopewa nafasi sahihi, huku akiwataka washiriki hao kuendelea kusambaza maarifa na uzoefu walioupata kwa vijana wengine nchini.

Kuhusiana na mada hii: