Tanzania na Urusi zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika maendeleo ya vijana kwa kuzingatia maeneo ya ruzuku, elimu, kilimo na teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Mnemba (Artificial Intelligence - AI).
Makubaliano hayo yalijadiliwa katika kikao cha pande mbili kati ya Mkuu wa Wakala wa Shirikisho la Masuala ya Vijana wa Urusi (Rosmolodezh), Grigory Gurov, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana Mhe. Joel Nanauka, Joel Arthur Nanauka, na Balozi wa Tanzania nchini Urusi Mhe Fredrick Kibuta pembeni mwa Tamasha la Kimataifa la Vijana (IFY 2026) linaloendelea jijini Ekaterinburg.
Akimkaribisha Waziri Nanauka na ujumbe wake, Gurov alisema Urusi inaona umuhimu mkubwa wa kuendeleza mahusiano ya muda mrefu katika sekta ya vijana kati ya mataifa hayo mawili.

Alisema miaka miwili iliyopita imeonyesha kuwa vijana wa Urusi na Tanzania wana hamasa kubwa ya kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo, huku ushiriki wa vijana wa Tanzania katika tamasha hilo ukiwa ishara ya kuimarika kwa mahusiano hayo.
Katika mazungumzo hayo, upande wa Urusi uliwasilisha programu mbalimbali zinazotekelezwa kupitia Mradi wa Taifa wa Vijana na Watoto, ikiwemo mpango wa maendeleo ya miundombinu ya vijana, programu za kukuza ujasiriamali kwa vijana, mashindano ya utamaduni wa mitaani na michezo ya KARDO pamoja na tuzo za kimataifa za #WEARETOGETHER.

Eneo jingine lililopewa kipaumbele ni ushirikiano katika teknolojia za kisasa. Rosmolodezh pamoja na Kurugenzi ya Tamasha la Dunia la Vijana zitawezesha mawasiliano kati ya Tanzania na taasisi za serikali pamoja na kampuni za Urusi zinazojihusisha na maendeleo ya akili mnemba (AI) na teknolojia nyingine za hali ya juu.
Kikao hicho pia kilijadili upanuzi wa fursa za ruzuku kwa vijana wa Tanzania. Rosmolodezh imekuwa ikitoa msaada wa ruzuku kwa Watanzania wanaosoma na kuishi nchini Urusi, huku mazungumzo yakiendelea kuhusu uwezekano wa kupanua fursa hizo kwa vijana waliopo Tanzania.

Aidha, pande hizo mbili zimeendelea kujadili ushiriki wa vijana wa Tanzania katika vituo vya elimu vya vijana vinavyofanya kazi mwaka mzima katika maeneo mbalimbali ya Urusi. Tanzania imeonyesha nia kubwa ya kushiriki mafunzo na kubadilishana uzoefu hasa katika sekta ya kilimo.
Tamasha la Kimataifa la Vijana 2026 linafanyika Ekaterinburg kuanzia Septemba 11 hadi 17 chini ya kaulimbiu ya "Follow Your Dream", likiwakutanisha vijana 10,000 kutoka nchi 191 duniani, wakiwemo viongozi wa vijana, wajasiriamali, wataalamu wa teknolojia, wanasayansi, wanamichezo, wanahabari na wabunifu kutoka mabara mbalimbali.