Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

MAKAMU WA RAIS AZURU DAMPO LA PUGU KINYAMWEZI

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amefanya ziara katika Dampo la Pugu Kinyamwezi jijini Dar es Salaam, ambapo amekagua hali ya udhibiti na usimamizi wa taka. Katika ziara hiyo, ameambatana na viongozi wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, viongozi wa Ofisi yake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware Semesi, pamoja na baadhi ya watumishi wa taasisi hiyo.

 Mhe. Ndejembi amewaagiza viongozi wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, Wizara na taasisi husika kukutana na kujadili kwa kina njia bora na endelevu za kudhibiti taka katika dampo hilo. Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu miongoni mwa wadau hao ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazolikabili eneo hilo.

 Katika kutekeleza maagizo hayo, ameelekeza viongozi hao kufikia makubaliano kuhusu njia bora za udhibiti wa taka na kuwasilisha kwake ripoti yenye mapendekezo ndani ya siku saba. Aidha, ameagiza kupuliziwa dawa maalum dhidi ya vimelea vya magonjwa katika maeneo yanayolizunguka dampo, hususan makazi ya wananchi walio jirani, ili kupunguza hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoweza kusababishwa na taka.

 Sambamba na hilo, Makamu wa Rais amewataka viongozi na taasisi zinazohusika kushirikiana katika ukusanyaji na uwasilishaji wa takwimu sahihi za taka, ili taarifa zinazotolewa ziwe na uhalisia na kuendana. Amesema takwimu hizo ni muhimu kwa Serikali katika kupanga na kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na changamoto za taka, kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.

Kuhusiana na mada hii: