Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuimarisha utunzaji wa mazingira kuelekea mvua za El Niño, kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Akiongea na vyombo vya habari Leo, Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma NEMC Bi. Martha Kawishe amesema mvua ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa, lakini utupaji holela wa taka, kuziba kwa mifereji, ujenzi katika njia za asili za maji na uharibifu wa maeneo oevu vinaweza kuongeza hatari ya mafuriko. Maeneo ya mabondeni, kingo za mito, maeneo yenye miteremko na yenye mifumo duni ya kupitisha maji yanahitaji tahadhari zaidi.

Ameongeza kuwa Baraza limewataka wananchi kutotupa taka kwenye mifereji, mito na makorongo, huku Mamlaka za Serikali za Mitaa zikihakikisha njia za maji zinasafishwa na kubaki wazi. Aidha, NEMC imesisitiza kulindwa kwa kingo za mito, mabonde na maeneo oevu, pamoja na kuchukua hatua za kuzuia mmomonyoko wa udongo.
NEMC pia imewataka waendelezaji wa miradi, viwanda, vituo vya mafuta, migodi, hospitali na maeneo yanayohifadhi kemikali au taka hatarishi kuhakikisha vitu hivyo vinasimamiwa kwa usalama ili visisombwe na maji ya mafuriko na kuchafua vyanzo vya maji na makazi ya wananchi.
Baraza limesema litaendelea kushirikiana na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine katika kutoa elimu, ufuatiliaji na ukaguzi wa mazingira, pamoja na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya shughuli zinazoharibu mazingira. NEMC imewahimiza Watanzania kufuatilia taarifa rasmi za TMA na kuchukua hatua mapema, ikisisitiza kuwa kulinda mazingira ni hatua muhimu katika kupunguza athari za mvua kubwa na mafuriko.