Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuchangia ujenzi wa mifumo ya Akili Unde (AI) inayojumuisha lugha, utamaduni na mahitaji halisi ya jamii za Afrika, ili kuhakikisha kuwa Waafrika wanashiriki kikamilifu na kunufaika na fursa zinazotokana na maendeleo ya teknolojia hiyo.
Dhamira hiyo imeelezwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), wakati akizungumza katika mjadala wa ngazi ya juu uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81), jijini New York, Marekani.
Waziri Kairuki amesema Tanzania imeanza hatua za kuendeleza Jamii Large Language Model (JamiiLLM), mfumo wa Akili Unde unaolenga kuwezesha teknolojia hiyo kuelewa na kuhudumia jamii za Afrika kwa kuzingatia lugha, utamaduni, mazingira na mahitaji yao.
Amesema Kiswahili, ambacho ni miongoni mwa lugha zinazozungumzwa na watu wengi barani Afrika, kinatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya JamiiLLM, sambamba na juhudi za kujumuisha lugha nyingine za asili za Afrika.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha kuwa mapinduzi ya Akili Unde hayawaachi nyuma wananchi wetu kwa sababu ya lugha. Tunataka Mwafrika aweze kutumia na kunufaika na Akili Unde kupitia lugha anayoielewa, na wakati huo huo maarifa, lugha na mazingira ya Afrika yawe sehemu ya teknolojia inayojengwa kwa ajili ya dunia,” amesema Waziri Kairuki.
Ameeleza kuwa JamiiLLM inalenga kujumuisha lugha mbalimbali za Afrika, hatua hii itasaidia kupanua wigo wa matumizi ya Akili Unde katika elimu, afya, kilimo, huduma za Serikali, biashara na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, uwekezaji katika mifumo ya Akili Unde inayotambua lugha za Afrika ni muhimu katika kupunguza pengo la kidijitali na kuhakikisha kuwa maendeleo ya teknolojia yanakuwa jumuishi na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi, wakiwemo wale ambao hawatumii lugha zinazotawala mifumo mingi ya sasa ya Akili Unde.
Tanzania inaona maendeleo ya JamiiLLM kuwa sehemu ya safari pana ya kujenga uwezo wa Afrika katika Akili Unde, ambapo bara hilo halitakuwa soko na mtumiaji wa teknolojia pekee, bali pia mshiriki katika kubuni, kujenga na kuendeleza teknolojia inayozingatia lugha, utamaduni, maarifa na vipaumbele vya Waafrika.
Waziri Kairuki amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, vyuo vikuu, watafiti, wabunifu wa teknolojia na washirika wa maendeleo katika kujenga miundombinu, rasilimaliwatu, data na mifumo salama na yenye kuaminika itakayowezesha Afrika kutumia kikamilifu fursa za Akili Unde.
Amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi nyingine za Afrika na washirika wa kimataifa katika kujenga mazingira yatakayowezesha Akili Unde kuwa nyenzo ya kuchochea maendeleo jumuishi, kuongeza tija na kuboresha maisha ya wananchi.