Serikali ya Urusi imeidhinisha utaratibu maalum wa utoaji visa utakaowezesha wajumbe wa kigeni wanaoshiriki Tamasha la Kimataifa la Vijana (International Festival of Youth – IFY) 2026 kupata visa bila malipo.
Tamasha hilo, litakalofanyika mwezi Septemba 2026 katika mji wa Yekaterinburg chini ya mradi wa kitaifa wa Vijana na Watoto wa Urusi, linatarajiwa kuwakutanisha vijana viongozi 5,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani pamoja na mamia ya wageni waalikwa, waandishi wa habari, wanablogu na wawakilishi wa vyombo vya habari vya kimataifa.
Uamuzi huo umefikiwa kufuatia amri iliyotiwa saini na Waziri Mkuu wa Urusi, Mikhail Mishustin, ambaye ameielekeza Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi kutoa visa bila malipo kwa washiriki wote walioidhinishwa, wageni na wawakilishi wa vyombo vya habari watakaohudhuria tamasha hilo.

Kwa mujibu wa amri hiyo, visa hizo zitakuwa halali kuanzia Septemba 4 hadi Septemba 30, 2026, na kuwawezesha washiriki kushiriki kikamilifu katika programu kuu ya tamasha mjini Yekaterinburg pamoja na shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika maeneo tofauti ya Urusi.
Baada ya kukamilika kwa programu kuu ya tamasha hilo, washiriki 1,000 kutoka mataifa mbalimbali watapata fursa ya kutembelea mikoa mbalimbali ya Urusi ili kujionea kwa karibu tamaduni, mila na desturi, mafanikio ya maendeleo pamoja na upekee wa maeneo tofauti nchini humo.
Tamasha la Kimataifa la Vijana ni muendelezo wa Tamasha la Dunia la Vijana (World Youth Festival) lililofanyika katika mji wa Sirius kuanzia Machi 1 hadi 7, 2024, kufuatia agizo la Rais wa Urusi, Vladimir Putin, la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa miongoni mwa vijana. Tamasha hilo la mwaka 2024 liliwakutanisha vijana viongozi wapatao 20,000 kutoka nchi 190 duniani.
Kwa kuzingatia maelekezo ya Rais Putin ya kuhifadhi na kuendeleza mafanikio ya Tamasha la Dunia la Vijana, Urusi imeendelea kuandaa matukio ya kimataifa ya vijana kila mwaka. Mwaka 2025, Mkutano wa Tamasha la Dunia la Vijana ulifanyika katika mji wa Nizhny Novgorod na kuwashirikisha vijana 2,000 kutoka nchi 120.
Waandaaji wa tamasha hilo wameeleza kuwa Tamasha la Kimataifa la Vijana 2026 linatarajiwa kupokea washiriki hadi 10,000, huku Tamasha lijalo la Dunia la Vijana likitarajiwa kufanyika mwaka 2030 na kuwakutanisha washiriki 20,000 kutoka kote duniani.
Tamasha hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mazungumzo ya kimataifa, kubadilishana uzoefu wa kitamaduni na kuendeleza ushirikiano miongoni mwa vijana kutoka mataifa mbalimbali.