Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, Maria Zakharova, amesema kuwa ushirikiano wa kweli kati ya Urusi na nchi za Afrika unapaswa kujengwa kupitia watu, hususan vijana, ambao ndio msingi wa maendeleo ya baadaye ya mahusiano hayo.
Zakharova alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika kikao kilichoitwa "The African Vector: Straight Talk"kilichofanyika katika ukumbi wa mihadhara wa Dostoevsky, ambapo alieleza namna mazungumzo na ushirikiano kati ya Urusi na mataifa ya Afrika yanavyojengwa, maendeleo yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni na matarajio ya siku zijazo.

Katika mjadala huo, aligusia umuhimu wa kuimarisha mahusiano ya watu kwa watu pamoja na kuongeza fursa za ushirikiano katika elimu, utamaduni na maendeleo ya vijana.
“Iwapo tunataka ushirikiano wa kweli na Afrika, ni lazima uanze na watu wenyewe, na zaidi ya yote vijana,” alisema Zakharova.

Akihitimisha hotuba yake, aliwahimiza washiriki kuendelea kuweka mkazo katika elimu na kujijengea maarifa, akisisitiza kuwa mustakabali wa dunia uko mikononi mwa vijana wa kizazi cha sasa.
Kauli zake zimekuja wakati Urusi ikiendelea kuimarisha ushirikiano wake na mataifa ya Afrika kupitia majukwaa mbalimbali ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii, huku vijana wakitajwa kuwa nguzo muhimu katika kuendeleza mahusiano hayo kwa vizazi vijavyo.