Mzaliwa wa Ciudad Juarez, jiji la mpakani kaskazini mwa Mexico, Fierro, mwenye umri wa miaka 69, alitumia zaidi ya miongo minne gerezani nchini Marekani, akiwa amehukumiwa kifo katika jimbo la Texas kwa mauaji ambayo hakuyafanya.
Nusu ya muda huo aliutumikia peke yake kabisa, katika hali ya upweke uliomchosha akili na mwili.
"Haki imeninyang'anya kila kitu. Kama yamenikuta mimi, yanaweza kumkuta yeyote. Niko huru, lakini sina muda mrefu wa kuishi," anasema kwa sauti ya huzuni, akizungumza na BBC News Mundo kutoka chumba kidogo anachoishi juu ya paa la jengo jijini Mexico City.
Mwanzoni mwa miaka ya 1980, Fierro, ambaye wakati huo alikuwa akifanya kazi kama mchuma chili huko El Paso, alilazimishwa na kundi la maafisa wa polisi kutia sahihi hati ya kukiri mauaji ya dereva wa teksi, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Mexico (CNDH).
Aliachiliwa mwaka 2020. Mwaka huohuo, alianza kushirikiana na mtayarishaji wa filamu Santiago Esteinou kutengeneza "La libertad de Fierro" (2024) filamu ya waraka inayosimulia safari yake ya kuzoea maisha huru baada ya miaka 40 gerezani.
Chanzo: Nipashe